Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amepata afueni baada ya mahakama kusitisha ombi la kutaka abanduliwe mamlakani.

Akitoa uamuzi huo, hakimu Wamae Cherere alisema kuwa Bunge la Kaunti ya Meru halikufuata utaratibu mwafaka katika kuanzisha hoja hiyo.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Kawira amewaomba wawakilishi wadi wa kaunti hiyo msamaha na kuahidi kufanya kazi nao licha ya tofauti zao.

Mwangaza alifika kortini wiki jana akitaka kuagizwa kuzuiwa kwa Bunge la Kaunti kujadili ombi lake la kuondolewa madarakani. Kupitia kwa wakili wake Elias Mutuma, Gavana huyo alidai kuwa uchapishaji wa ombi la kumtimua uliitishwa na kutiwa sahihi na mtu asiyemfahamu katika bunge akikaimu kama karani.

Aidha aliambia mahakama kwamba bunge hilo lilithibitisha kuwa na mawazo yaliyoamuliwa sababu ya kuondolewa kwake ikizingatiwa kwamba wawakilishi wadi 68 kati ya 69 walikuwa wameidhinisha hoja hiyo.

Hoja ya kuondolewa kwake iliwasilishwa na mwakilishi wadi wa Abogeta Magharibi Dennis Kiogora, ambaye pia ni karani wa Walio wachache bungeni mnamo Novemba 21.

November 30, 2022