Mahakama imeahirisha kwa muda wa wiki tatu kesi ya ufisadi ya shilingi bilioni 7.4 dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na wengine kufuatia ombi la kuangazia suala hilo.Hatua hii inajiri baada ya mahakama kuelezwa kuwa Gachagua alimwandikia barua mkurugenzi wa mashtaka ya umma ili kesi yake ikaguliwe.

Kesi hiyo iliorodheshwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa siku tatu lakini washtakiwa hawakufika binafsi mbele ya mahakama Jumatatu asubuhi.Hata hivyo, mawakili wake waliambia mahakama kuwa hawakufahamu iwapo kesi hiyo ingesikizwa mtandaoni au ana kwa ana.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma iliiomba mahakama kuipa muda zaidi wa kupitia upya kesi, ikibaini kuwa imepokea barua nyingi za kutaka mapitio.Gachagua anadaiwa kujipatia kwa njia ya ulaghai shilingi bilioni 7.4 kama mapato ya uhalifu kati ya mwaka 2013 na 2020 kupitia shughuli za kibiashara serikalini.

Gachagua Anakabiliwa na mashtaka sita kati ya hayo yakiwamo kujipatia mali ya umma kwa njia ya udanganyifu, mgongano wa kimaslahi miongoni mwa mengine.Gachagua anashtakiwa pamoja na aliyekuwa meneja wa CDF Mathira William Mwangi Wahome, Ann Nduta Ruo, Jullianne Jahenda Makaa,Samuel Murimi Ireri, Grace Wambui Kariuki, Lawrence Kimaru, Irene Wambui Ndigiriri, David Reuben Nyangi na kampuni ya Rapid Medical Supplies Ltd.Tisa hao kwa pamoja wanashtakiwa kwa njama ya kutekeleza hatia ya ufisadi kwa kudaiwa kulaghai Serikali ya Kaunti ya Nyeri shilingi milioni 27.4 ili kusambaza mashine za kusafisha damu kwa Hospitali rufaa ya Nyeri.

October 17, 2022