Zoezi la kuwapiga msasa mawaziri ishirini na wawili walioteuliwa na rais William Ruto limeng’oa nanga hivi leo katika majengo ya bunge.Musalia Mudavadi ambaye ameteuliwa kama mkuu wa mawaziri alikuwa wa kwanza kupigwa msasa ambapo ameelezea baadhi ya mabadiliko aliyoleta kwenye wizara ya hazina ya kitaifa wakati wa utawala wa rais mstaafu hayati mzee Mwai Kibaki. Aidha Mudavadi amesema kuwa hakuna mgongano wowote kati ya majukumu ya mkuu wa Mawaziri na Naibu rais.

Wa pili kupigwa msasa ni aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi ambaye ameteuliwa kuwa mwanasheria mkuu.Kuhusiana na suala la kuondolewa kwa kesi za ufisadi mahakamani, Muturi amedokeza kuwa ni jukumu la mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuanza, kuchukua na kuondoa mashtaka ya jinai isipokuwa kesi ambazo zipo mbele ya mahakama ya kijeshi.

Mwingine ambaye amepitia zoezi hilohilo ni waziri mteule wa ulinzi Aden Duale ambaye ameahidi kuwaunganisha na kuwalinda wakenya iwapo ataidhinishwa kama waziri. Wengine watakaopigwa msasa leo ni pamoja na  waziri mteule wa mambo ya kigeni Alfred Mutua na kisha baadaye waziri mteule wa maji na usafi Alice Wahome.

Kwa mujibu wa karani wa bunge la kitaifa Sarah Kioko ni kwamba zoezi hilo litaendelea hadi Jumamosi, Oktoba 22, isipokuwa siku ya Alhamisi, Oktoba 20, ambapo nchi itaadhimisha Siku ya Mashujaa.

October 17, 2022