Kaunti ya Narok ndio mwenyeji wa awamu ya 42 ya michezo ya Kenya Communications Sports (KECOSO).Michezo hiyo ambayo imeandaliwa katika uga wa Ole Ntimama imeng’oa nanga hii leo na itakamilika tarehe 26 mwezi huu wa agosti.

Kulingana na katibu mkuu wa KECOSO Omole Asiko, baraza tawala lilichagua Narok kwa kuzingatia vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na uwepo wa hoteli za kuwakaribisha maafisa na washiriki na mipango ya ulinzi na usalama.

Aliongeza kuwa Narok ilishinda kaunti za Nakuru, Eldoret, Nyeri, Kirinyaga, na Meru na itakuwa  ikiandaa michezo hiyo ya kila mwaka.

Mashindano ya mwaka huu yatashirikisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, gofu, snooker, kuogelea, mpira wa vikapu, mpira wa miguu, dati, pool, scrabble, voliboli, netiboli na tenisi ya meza.

Kecoso ilianzishwa mwaka 1978 na huleta pamoja mashirika ya serikali chini ya wizara za Barabara na Uchukuzi, Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali na Michezo.

August 19, 2023