Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imesema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitashuhudiwa katika muda wa wiki moja ijayo ambapo walioathiriwa na mafuriko huenda wakaathirika Zaidi kutokana na mvua hizo.

Katika taarifa ya kila wiki ya hali ya hewa, mkurugenzi wa idara hiyo Dkt David Gikungu amebainisha kuwa mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi huku dhoruba zikitarajiwa kutokea katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu, Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Kusini-Mashariki, Nyanda za chini, Pwani na Kaskazini-mashariki mwa Kenya.

Kulingana na Gikungu, mvua iliendelea kurekodiwa katika maeneo mengi ya nchi katika muda wa wiki moja iliyopita huku dhoruba zikitokea katika kaunti kadhaa zikiwemo Makueni, Isiolo, Meru, Laikipia, Kitui, Machakos, Tharaka Nithi, Taita Taveta, Embu na Garissa.Kulingana na ripoti hiyo pia kupungua kwa viwango vya mvua katika ukanda wa Pwani, Kaskazini Mashariki na Kaskazini-magharibi mwa Kenya kulirekodiwa katika kipindi hicho ikilinganishwa na wiki iliyopita.

Utabiri wa hivi punde unakuja kufuatia uharibifu katika sehemu za nchi unaotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika sehemu kubwa ya nchi.

 

November 14, 2023