Mwanamke mmoja katika kaunti hii ya Narok ameshtakiwa kwa madai ya kumnajisi mvulana mwenye umri wa 15, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili.

Mary Njoki aliyefikishwa mbele ya hakimu mkuu Rosalinda Shinyanda, anadaiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Januari 4 mwaka huu katika mtaa wa Fanaka viungani mwa mji wa Narok.

Mshukiwa huyo anasemekana kumnajisi mtoto huyo kwa kugusana na pia kumshika sehemu zake za siri.Mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kumnyima mshukiwa dhamana kwa madai kuwa yeye ni jamaa wa mtoto huyo na huenda mzozo ukazuka kati yao.

Upande wa mashtaka pia uliiomba mahakama kuharakisha upelelezi na uamuzi ili kuwapa wazazi nafasi ya kuwasilisha ushahidi.

Mbali na kesi hiyo, mwanamume mmoja vilevile alishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na uuzaji wa nyama ya wanyamapori bila kuwa na leseni jambo ambalo ni kinyume cha katiba kwa mujibu wa kifungu cha 98(1) cha uhifadhi wa wanyamapori cha mwaka 2013. Konene Sordo alinaswa na kilo 170 za nyama ya pundamilia mnamo Januari 10, 2023 huko Septai Narok Kusini.

January 24, 2023