Mwenyekiti anayeondoka wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC Wafula Chebukati amekabidhi ripoti yake ya mwisho kwa rais William Ruto huku muda wake ukikamilika rasmi.

Hafla ya makabidhiano ilifanyika hii leo katika Ikulu ya Nairobi. Taasisi zingine 15 ambazo zilishirika katika mchakato wa kuandaa uchaguzi uliopita vilevile zilikabidhi ripoti zao za kuondoka. Bw Chebukati alikabidhi ripoti hiyo kwa niaba ya baraza zima la uchaguzi, pamoja na ripoti ya tathmini ya baada ya uchaguzi ambayo ilizinduliwa Jumatatu.

Mwenyekiti huyo alikariri kuwa ameridhika na jinsi alivyoendesha uchaguzi wa Agosti 2022 na kwamba wameweka msingi kwa timu inayokuja na ambayo itaendesha uchaguzi ujao.

Aidha alionyesha matumaini kuwa tume hiyo itasalia imara chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji Hussein Marjan na timu inayoingia ya makamishna.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula na Spika wa Seneti Amason Kingi.

Chebukati anaondoka pamoja na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu.

January 17, 2023