Polisi nchini Zambia wamegundua miili 27 ya watu wanaodhaniwa kuwa wahamiaji waliongia nchini humo kinyume cha sheria kutoka Ethiopia na Somalia.

kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Danny Mwale,mtu mmoja alikuwa bado yu hai wakati alipopelekwa hospitalini. Sababu hasa ya vifo vya watu hao haijafahamika, lakini inafikiriwa huenda walikosa hewa wakati wakisafirishwa.

Zambia imekuwa ikipambana na biashara haramu ya binadamu kwa miaka kadhaa sasa. Kulingana na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Zambia imechukua wakimbizi zaidi ya 100,000 kutoka mataifa jirani ya Kongo, Burundi, Angola na Rwanda. Kwa viwango vya eneo la kusini mashariki mwa Afrika, nchi hiyo inachukuliwa kuwa tulivu zaidi kisiasa.

Hata hivyo, Zambia inapambana na kiwango kikubwa cha umasikini na utapiamlo na pia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

December 12, 2022