Gavana wa Kaunti ya Narok Patric Ntutu ameahidi kuimarisha usalama wa wanyamapori katika kaunti ya Narok, ili kusaidia kuinua mapato yanayotokana na utalii.

Katika hotuba yake wakati akiongoza maadhimisho ya shamrashamra za jamhuri katika eneo la Olderkesi, Eneobunge la Narok magharibi, Gavana huyo amesema kuwa serikali yake imepata kupigwa jeki na kupata silaha za kisasa zitakazosaidia katika kukabiliana na kero la majambazi na wawindaji haramu.

Ntutu pia amesema kuwa serikali ya kaunti ya Narok imetoa ardhi ya kujenga ofisi ya uhamiaji eneo la Olpusimorou Narok magharibi akipania kuimarisha biashara na uwiano kati ya mataifa ya Kenya na Tanzania.

Kauli yake imeungwa mkono na Kamishna wa kaunti ya Narok Bw. Isaac Masinde, ambaye ameahidi kukamilisha uchunguzi na kuwakamata wanaojihusisha na kuwaua wanyama pori, akiweka wazi kuwa ndovu 5 na twiga 3 wameuwawa katika mbuga ya kitaifa ya Maasai Mara.

Viogozi mbali mbali akiwemo mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Togoyo, mbunge wa Narok kusini Kitilai Ntutu, mbunge wa bunge la Africa mashariki David Sankok, kiongozi wa kina mama katika kaunti ya Narok Rebecca Tonkei, spika wa bunge la kaunti ya Narok Davis Dikirr miongoni mwa wengine pia walihudhuria sherehe hizo.

December 12, 2022