Maafisa wa polisi hapa Narok wanachunguza kisa ambapo kamanda wa polisi wa Narok ya kati Fredrick Shiundu alitekwa nyara na watu wasiojulikana kwenye lango la kuingia kwake mwendo wa saa nne usiku wa kuamkia leo.

Kamanda wa polisi wa Narok Kizito Mutoro akidhibitisha hayo amefichuwa pia wahalifu hao walimnyanganya afisa huyo bunduki yake aina ya Jericho na ambayo ilikuwa na risasi 14 na wakamsafirisha hadi eneo la Tipis walikomuacha akiwa ndani ya gari.

Kizito kadhalika amesema baada ya kupata taarifa hizo za afisa huyo kutekwa nyara kutoka kwa mke wake walianza kumtafuta na wakafanikiwa kumpata eneo hilo la Tipis mwendo wa saa tisa asubuhi.Kamanda huyo wa polisi vilevile ametaja baadhi ya mambo ambayo wanachunguza ili kubaini kile ambacho kilichochea watu hao kuchukuwa hatua hiyo.

Haya yanajiri baada ya afisa huyo kuongoza oparesheni mjini Narok wikendi iliyopita ambapo alinasa bhangi yenye dhamani ya shilingi milioni 1.8 na mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 23 kutiwa mbaroni katika mtaa wa Total vungani mwa mji wa Narok.

February 8, 2023