BY ISAYA BURUGU 15TH AUG 2023-Aliyekuwa Mbunge wa kwanza wa Budalang’i baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru James Charles Nakhwanga Osogo ameaga dunia.

Osogo alihudumu kama waziri na waziri msaidizi katika serikali ya hayati marais Jomo Kenyatta na Daniel Moi.

Alizaliwa mwaka 1932, katika kijiji cha Bukani, Wilaya ya Bunyala , kaunti ya Busia. Alisomea taaluma ya uwalimu katika chuo cha waalimu cha Kagumo na kuhitimu kama mwalimu daraja la P2 na kuhudumu kama mwalimu katika shule mbali mbali.

Alichaguliwa mbunge wa Busia Kusini mwaka 1963 na kuteuliwa waziri msaidizi wa Kilimo kati ya mwaka 1964-1966. Baadhi ya wizara ambazo alihudumu kama waziri ni kama ifyatavyo.

1966-1969 Waziri wa Habari na Utangazaji.

1969-1973 Waziri wa Biashara na Viwanda.

1973-1974 Waziri wa Serikali za Mitaa.

1974 Waziri wa Afya; wakati huo huo waziri wa Mambo ya Nje.

1978 Naibu kiongozi wa shughuli za Serikali.

1979 Waziri wa Kilimo.1

980 Waziri wa Mifugo.

Mbunge wa Budalang’i Raphael Wanjala akimuomboleza  marehemu  amemtaja kama kiongozi aliyejitolea kutumikia jamii.

“Marehemu James aliigusa vyema jamii yetu akiiweka Budalangi kwenye mwelekeo mzuri wa maendeleo ambao ulihamasisha watu kama mimi kuchukua changamoto na kusaidia kutetea mabadiliko zaidi kwa kuchanganya falsafa zake na zile za marehemu Peter Okondo katika uongozi wangu,” Wanjala alisema.

Mbunge huyo aliendelea kusema kuwa alifanya kazi kwa karibu na Osogo kabla ya uchaguzi wa 1997.

“James alikuwa kiongozi ambaye alitafuta ushauri kutoka kwa wote, alipokea ukosoaji kwa uzuri na hakuwa na kinyongo hata kidogo. Kwa miaka mingi hata tulipotofautiana katika mambo ya siasa uhusiano na urafiki wetu haukuwahi kuathiriwa kwa namna yoyote na familia zetu zimeendelea kuishi pamoja kama kaka na dada”, Wanjala aliongeza.

 

Share the love
August 15, 2023