Uganda imetangaza kuwa virusi vya ebola vilivyoibuka karibu miezi minne iliyopita na kuua watu 55 vimeisha nchini humo,tangazo ambalo limeungwa mkono na shirika la afya duniani WHO.

Kwa mujibu wa wawziri wa afya nchini humo Jane Aceng ni kwamba Januari 11 iliadhimisha siku 113 tangu kuanza kwa mlipuko wa Ebola ambayo husababisha kuvuja damu. Katika muda huo, Uganda ilithibitisha jumla ya visa 142, vifo 55 huku wagonjwa 87 wakipona.

Kulingana na WHO, mlipuko wa ugonjwa huo unaisha wakati hakuna kesi mpya kwa siku 42 mfululizo mara mbili ya kipindi cha incubation cha Ebola.

Mlipuko wa Uganda ulisababishwa na virusi vya Ebola vya Sudan, mojawapo ya aina sita za virusi vya Ebola ambavyo kwa sasa hakuna chanjo.

Aidha kuna chanjo tatu zinazojaribiwa nchini Uganda, hizi  ni pamoja na chanjo iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford na Taasisi ya Jenner nchini Uingereza, nyingine kutoka Taasisi ya  chanjo ya Sabin nchini Marekani, na ya tatu kutoka kwa Mpango wa Kimataifa wa Chanjo ya UKIMWI (IAVI).

January 11, 2023