Waziri wa usalama wa Ndani Kithure Kindiki ameangazia maendeleo ambayo wizara yake imefanya katika vita dhidi ya uhalifu katika eneo la North Rift.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uwiano wa Kitaifa, Waziri huyo alisimulia jinsi ukosefu wa usalama ulivyolemaza shughuli za masomo katika eneo hilo.

Kulingana na Kindiki, mhalifu mmoja alihamia katika mojawapo ya shule ambazo zilikuwa zimefungwa baada ya ugaidi kuzuka na kuigeuza kuwa nyumba yake.

Waziri huyo alisema kufikia sasa, serikali imefungua tena shule 14 kati ya 21 zilizokuwa zimefungwa.

Aliongeza kuwa baadhi ya shule zimeaharibiwa na wahalifu na kuziteketeza huku wizara yake ikishirikiana na Wizara ya Elimu kujenga madarasa mapya. Kaunti zilizoathiriwa zaidi ni Baringo, Samburu, Turkana na Elgeyo Marakwet.

Kwingineko ni kwambawahalifu walivamia tena wakaazi wa Marsabit na kuua watu watatu mwendo wa alfajiri.

Wahalifu hao walifanya mashambulizi katika eneo la Hallan, Kargi licha ya oparesheni ya kijeshi iliyoanzishwa na serikali.

Wavulana wawili wenye umri wa kati ya miaka 5 na 7 na mwanamume wa makamo ndio waliouwawa. Aidha mwanamume mwingine mmoja anauguza majeraha mabaya kutokana na shambulio hilo ambalo limewatia wakaazi hofu.

Chifu msaidizi wa eneo hilo Moses Galoro alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa idadi isiyojulikana ya mbuzi na kondoo pia waliibiwa.

March 1, 2023