Serikali kuu imeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana akiwadhalilisha wanafunzi msimu huu wa utalii, hasa katika maeneo ya karibu na hifadhi na vivutio vya kitalii. Onyo hilo limetolewa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Narok Magharibi, Bw. Joseph Mtile Lewa, alipohutubia wananchi katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika zilizofanyika katika uga wa shule ya Leshuta Comprehensive.
Akizungumza baada ya maandamano ya amani yaliyoanzia katika kituo cha biashara cha Leshuta, Bw. Lewa alisisitiza kuwa serikali haitavumilia visa vya dhuluma za kingono, ndoa na mimba za mapema vinavyowakumba wasichana hasa katika maeneo ya utalii, na kuongeza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa wote watakaopatikana na hatia.
Kauli yake iliungwa mkono na Dkt. Samuel Manoti Masese, Mkurugenzi wa Huduma za Watoto katika eneo la Bonde la Ufa, ambaye alionya kuwa adhabu ya hadi miaka 10 gerezani inamngoja yeyote atakayekiuka haki za watoto. Alihimiza wadau wote kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao katika kulinda watoto dhidi ya dhuluma.
Naye Dkt. Evans Osumba, Meneja wa Shughuli za Shirika la World Vision kwa kaunti za Narok, Bomet na Kericho, aliwataka walimu kote nchini kuimarisha utaratibu wa kuchukua mahudhurio ya wanafunzi kila siku kama njia mojawapo ya kudhibiti visa vya kutoweka kwa wanafunzi au kujiingiza katika mazingira hatarishi.
Sherehe za mwaka huu zilibeba kaulimbiu: “Planning and Budgeting for Children’s Rights and their General Wellbeing” na zilihudhuriwa na wazazi, wanafunzi, maafisa wa watoto pamoja na wawakilishi kutoka makampuni mbalimbali ya kitalii eneo hilo.
Ripoti zinaonyesha kuwa dhuluma za kingono dhidi ya wasichana wa shule, hasa maeneo ya karibu na vivutio vya kitalii, zimeendelea kuwa changamoto kubwa. Watalii wengine hutoa ahadi za uongo kwa wasichana hao na kuishia kuwaingiza katika ndoa za mapema, mimba zisizotarajiwa na kukatisha masomo yao, hasa kwa wanaotoka katika familia zisizojiweza.