Zaidi ya lita milioni 2.8 za pombe haramu zimekamatwa na zaidi ya washukiwa 900 wamekamatwa tangu Serikali ilipoanzisha msako wa kitaifa mnamo Desemba 2025, Wizara ya usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa imesema.
Kulingana na data iliyokusanywa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya, Idara ya makosa ya Jinai (DCI) na mashirika ya usalama wa mipaka, operesheni hiyo pia imeshuhudia kukamatwa aina mbalimbali za dawa za kulevya.
Msako huo ulifuatia agizo lililotolewa na rais William Ruto mnamo Desemba 31, 2025, alipotangaza matumizi mabaya ya pombe haramu na dawa za kulevya kuwa tishio kwa maendeleo ya kitaifa na usalama.
Mamlaka ziliripoti kupatikana kwa lita 21,280 za ethanoli, kilo 4,347 za bangi, kilo 7.7 za kokeini, kilo 6.4 za ketamine na kilo 1.1 za methamphetamine.
Tangu wakati huo, Wizara ya usalama wa ndani imeanzisha kampeni ya mashirika mengi inayoongozwa na NACADA kwa ushirikiano na Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Maafisa Tawala wa Serikali ya Kitaifa.
Data rasmi inaonyesha kwamba lita 2,846,590 za pombe haramu zilikamatwa katika kipindi kinachopitiwa, huku eneo la Bonde la Ufa likirekodi idadi ya juu ya zaidi ya lita 870,000.

