Rais William Ruto ameongoza hafla ya kuwapa bendera ya taifa na kuwatuma wanajeshi wa kenya katika taifa la Kidemokrasia la Congo, kusaidia taifa hilo katika vita dhidi ya kundi la waasi wa M23, kama mojawapo ya juhudi za Pamoja za mataifa ya afrika mashariki za kutuma kikosi cha kijeshi katika taifa hilo ili kurejesha amani.

Rais Ruto amesema kuwa taifa la Kenya limejitolea katika kushirikiana na mataifa ya ukanda wa Afrika mashariki ili kuinua ustawi wa ukanda huu hasa mataifa yanayokumbwa na misukosuko. Jeshi la kenya limeungana na wanajeshi kutoka mataifa jirani katika kikosi cha pamoja cha Majeshi ya ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) Kikosi hicho kinajumuisha wanajeshi kutoka Uganda, Sudan Kusini, Kenya na hata taifa la Rwanda.

Aidha rais pia aliwaombea wanajeshi hao baada ya kuwakabidhi rasmi bendera ya taifa kama njia ya kuwatuma rasmi katika shughuli hizo za kuweka amani, katika taifa hilo ambalo limekua katika hali ya misukosuko hasa kutokana na kero la waasi wa kundi la M23.

November 2, 2022