Moto sokoni Gikomba

Wachuuzi katika soko la Gikomba walikumbwa kwa mara nyingine na mkasa wa moto Jumamosi 15.10.2022, baada ya moto mkubwa kuteketeza sehemu ya soko hilo. Hata ingawa idara ya kukabiliana na mikasa katika jiji la Nairobi ilifanikiwa kuudhibiti moto huo, wachuuzi wa Gashosho na soko la samaki kwenye soko hilo waliachwa wakihesabu hasara kubwa.

Mbunge wa Kamukunji Yussuf Hassan sasa amewataka Rais William Ruto pamoja na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kutangaza soko la Gikomba kuwa eneo hatari na la maafa, baada ya ongezeko la mikasa hii ya mara kwa mara.

 Mbunge huyo pamoja na viongozi wengine katika kaunti ya Nairobi walizuru soko hilo, kuwatembelea wachuuzi na kudadisi madhara yaliyosababishwa na tukio hilo la asubuhi.

Mkasa huo wa hivi karibuni kulikumba soko hilo uliteketeza sehemu ya soko la Gashosho na soko la samaki wakavu kabla ya kusambaa katika maeneo ya Gorofani na Bondeni ambayo yanapakana na soko hilo. Wachuuzi katika soko hilo wameendelea kutoa kauli mseto kuhusu mkasa huo wakieleza kuwa wamepokea ahadi za kusaidiwa kuzuia mikasa hii jambo ambalo halijatiliwa maanani.

October 15, 2022