Watu wanaodaiwa kuwa wanamgambo wamewaua watu 12 kwa kuwakatakata kwa mapanga katika kijiji kimoja Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikumbwa na machafuko kutoka kwa makundi yaliyojihami kwa silaha.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, kiongozi wa shirika moja la kiraia katika eneo hilo, Gustave Kakani amesema watu hao, walikivamia kijiji cha Masome jimboni Ituri jana asubuhi na kufanya uovu huo, ambapo wanawake na wanaume waliuwawa kwa kupigwa mapanga.

Baadhi ya miili ilipatikana ikiwa imekatwa viungo huku baadhi ikiwa imefungwa mikono. Kakani amesema wahanga walipitia mateso makubwa kabla ya kuuwawa. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na shambulio hilo. Kundi la waasi wa ADF ndilo kundi baya zaidi kati ya makundi zaidi ya 120 ya wanamgambo yanayowahangaisha wakaazi wa Mashariki mwa Congo.

October 15, 2022