Kinara wa azimo la umoja Raila Odinga amesema kuwa hatua ya serikali kuanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa tisa wa kitengo cha SSU kilichovunjwa, inanuia kumdhalilisha aliyekuwa mkurugenzi wa DCI George Kinoti. Kwenye kikao na waandishi wa habari, Odinga amedokeza kuwa iwapo serikali imeamua kufuatilia kesi za mauaji basi inastahili kuangazia pia kesi za wafanyakazi wa serikali waliouwawa kwa njia tatanishi kama vile Jacob Juma na Chris Msando.

Kuhusiana na suala la ushuru, Raila ameishutumu serikali kwa kutoa pendekezo la kuwaongezea wakenya ushuru ili kufanikisha ahadi walizotoa wakati wa kampeni.

Hali kadhalika muungano huo umemtambulisha Wafula Wamunyinyi kuwa mpeperushaji bendera wake katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Bungoma.Odinga amesema kuwa tayari muungano huo umempatia Wamunyinyi cheti cha uteuzi huku akielezea Imani kuwa atashinda kwenye uchaguzi huo. Kiti cha useneta wa Bungoma kilisalia wazi baada ya Moses Wetangula kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC inatazamiwa kuendesha uchaguzi huo mdogo tarehe nane Disemba.Katika tarehe hiyo hiyo, tume hiyo pia itaendesha uchaguzi mdogo katika Wadi za Ololmasani, Kyome/Thaana, Utawala, Mumias Kaskazini na Gem kusini.

November 3, 2022