Shirika la afya duniani WHO limesema janga la covid-19 pamoja na vita na migogoro ni masuala yaliyorudisha nyuma juhudi za kuimarisha afya na ustawi wa wanawake pamoja na watoto. Kwa mujibu wa data za WHO zilizowasilishwa katika mkutano wake wa kilele mjini Berlin, njaa pamoja na umasikini ni mambo yaliyoongezeka na kuna dalili za wazi za ongezeko la ndoa za mapema,unyanyasaji na matumizi ya nguvu majumbani pamoja na maradhi ya msongo wa mawazo na kiwewe miongoni mwa watu wenye umri wa balekhe.

Data hiyo vilevile imeonyesha kuwa takriban watoto milioni 21 duniani walikosa chanjo katika mwaka 2021, idadi ambayo ni milioni 6 zaidi ya ile iliyoshuhudiwa mwaka 2019 kabla ya janga hilo kuzuka. WHO imesema ulimwengu hauko kwenye nafasi ya kuyaafikia malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 ambayo ni pamoja na afya, lishe bora na elimu miongoni mwa mengine.

October 18, 2022