Vijana

Kiongozi wa taifa Rais William Ruto, amewataka vijana kukumbatia nafasi za ajira zinazopatikana kwenye mifumo ya kidijitali, na kujipatia kipato cha kuimarisha maisha yao ya siku kwa siku.

Akizungumza katika hafla ya Youth Connect Africa Katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi, kiongozi wa taifa ameeleza haja ya ulimwengu kukumbatia uwepo wa nafasi za ajira za mkondoni, akiongeza kwamba ipo haja ya taifa la Kenya kubuni sheria mpya zitakazoongoza utendakazi wa kidijitali ili kuwawezesha vijana kujitosa kwenye kazi hizi.

Rais Ruto vilevile ameeleza kwamba wizara ya Elimu nchini inashirikiana na kampuni ya kiteknolojia ya Google katika kufanikisha mpango wa kutoa mafunzo ya kutengeneza programu mifumo ya kidijitali katika shule za msingi na upili humu nchini.

Kiongozi wa taifa amesema vijana katika taifa la Kenya na bara la Afrika hawana budi ila kukumbatia teknolojia. Viongozi mbalimbali pia walihudhuria hafla hiyo akiwemo naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

December 9, 2023