Jopokazi la wanachama 42 lililoteuliwa na Rais William Ruto kutathmini mfumo wa Elimu nchini na kutoa mapendekezo litaanza kuendesha vikao vya ushiriki wa umma mnamo Jumanne, Novemba 1. Kulingana na Mwenyekiti wa jopo hilo Prof. Raphael Munavu, zoezi hilo litaendeshwa katika kaunti 47 kuanzia saa 8 asubuhi hadi saa 10 asubuhi.

Mnamo Novemba 1, kamati hiyo itaendesha zoezi hilo katika kaunti za Kwale, Taita Taveta, Marsabit, Nyandarua, Turkana, Kericho, Busia, Migori, Mandera na Samburu. Tarehe 3 Novemba jopo hilo litazuru baadhi ya shule za upili za Mombasa, Makueni, Nyeri, Elgeyo Marakwet, Bungoma, Nyamira na Homa Bay.

Baada ya hapo,zoezi hilo litaendelea Novemba 4 katika Kaunti za Isiolo, Wajir na Laikipia.Mnamo Jumatatu, Novemba 7, zoezi hilo litaendelea katika Kaunti za Kilifi, Kitui, Kirinyaga, Bomet, Trans Nzoia, Kakamega na Kisii kabla ya jopo hilo kuwashirikisha wakazi wa kaunti za Meru, Garissa na Baringo mnamo Novemba 8.

Kamati hiyo vile vile itashirikisha wadau husika wa elimu katika kaunti za Lamu, Embu, Muranga, Pokot Magharibi, Narok, Nandi na Siaya. Zoezi hilo litakamilika katika kaunti za Tana River, Machakos, Tharaka Nithi, Kiambu, Uasin Gishu, Kajiado, Vihiga, Kisumu, Nairobi na Nakuru mnamo Novemba 11.

October 28, 2022