Bunge la Kitaifa alasiri ya leo limeidhinisha majina ya wanachama wake wa Kamati ya shughuli za Bunge, tayari kwa kuanza rasmi kwa shughuli za bunge hilo siku ya kesho. Spika Moses Wetangula amewaagiza wanakamati hao kuanza shughuli zao mara moja, kuanda hoja na miswada ambayo itaanza kujadiliwa katika kikao cha kesho.

Kisheria, Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge ina jukumu la kupanga shughuli zitakazotekelezwa Bungeni ambayo ina hakikisha kuwa shughuli Bunge hazitalemazwa. Samuel Chepkonga (Ainabkoi), Faith Gitau (Mwakilishi wa Wanawake Nyandarua), Omboko Milemba (Emuhaya) watawakilisha Muungano wa Kenya Kwanza.

Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Alliance utawakilishwa na Robert Mbui (Kathiani), TJ Kajwang (Ruaraka), Adan Keynan (Eldas), Sarah Korere (Laikipia Kaskazini) na Joshua Mbithi (Masinga).

Wengine watakaohudumu kwenye katati hiyo ni pamoja na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi (Ugunja), Kinara wa Wengi Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini), na Kinara wake wa Wachache Junet Mohammed (Suna Mashariki).

October 11, 2022