Waziri wa uchukuzi nchini, ameishtumu kampuni ya ndege ya KLM yenye makao yake nchini Uholanzi, kwa kile alichokiita nia ya kuzua hofu kati ya wakenya na pia kati ya mataifa mengine kuhusu hali ya usalama nchini.

Shutma za Waziri Murkomen zinajiri baada ya kampuni hiyo ya usafiri wa ndege kuchapisha notisi kwa wateja wake kuwa safari zao kuja Kenya zitashuhudia hitilafu, kutokana na machafuko ya ndani kwa ndani katika taifa la Kenya.

Hata hivyo kampuni hiyo imechapisha ombi la kuomba msamaha na kusema kuwa notisi hizo zilichapishwa bila kukusudia kwani zilifaa kuwaendea wateja wake katika taifa Jirani la Tanzania.

Waziri Murkomen ameeleza kusikitishwa na kosa hilo na kueleza kuwa lingesababisha hasara kubwa kwa uchumi wa taifa.


Awali ubalozi wa Uholanzi nchini, ulitupilia mbali taarifa zilizokua zikienea kuhusu kukatishwa kwa ziara za kutoka na kuingia katika taifa la Kenya, ukisema kuwa hakuna tangazo la aina hiyo lililotolewa na ubalozi huo.

Taarifa kutoka kwa kampuni ya usafiri wa ndege ya KLM, kuomba msamaha kwa taifa la Kenya kwa chapisho la awali kuhusu kusitishwa kwa safari za ndege za kampuni hiyo humu nchini.
Picha ya skrini ya mtandao wa kampuni ya ndege ya KLM ikionyesha ujumbe kuwa Kenya imeorodheshwa kati ya mataifa ambayo safari za ndege katika kampuni hiyo zitasitishwa.

 

January 28, 2023