Wenyeji wa kaunti ya Narok  wametakiwa kuhakikisha kuwa swala la ukeketaji linatokomezwa kikamilifu.Wito huu umetolewa huku Kenya ikiungana na ulimwengu hii leo kuadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani.

Kwa mujibu wa Mihele Kishoyian ambaye ni mwanaharakati wa kupigania haki za mtoto wa kike amesema wakati umefika kwa serikali kukaza Kamba  dhidi ya watu wanaoendeleza mila zilizopitwa na wakati na ambazo ni vikwazo kwa ustawi wa mtoto wa kike kielimu na kijamii.

Maadhimisho haya yanafanyika wakati serikali mpya inaanza jukumu lake la kuwahudumia wananchi katika muda wa miaka mitano ijayo.Jukumu la utunzaji mtoto wa kike linatarajiwa kupewa kipau mbele huku wanaharakati wa kutetea mtoto wa kike wakitarajia kuona mikakati itakayowekwa kulinda na kutetea haki za mtoto huyo.

Changamoto zinazomtatiza mtoto wa kike katika kuafikia azma yake maishani ni Pamoja na ndoa  za mapema ,umasakini na Maisha magumu.

Kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya leo wawakilishi wa makundi tofauti yanayotetea haki za mtoto wa kike yanataka mtoto wa kike kuhusishwa kikamilifu katika serikali za kaunti na ile ya kitaiafa ili kupigania haki zao. Mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea ukame pia yanasemekana kuwaathiri Watoto wa kike.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Wakati wetu ni sasa – haki zetu, maisha yetu ya baadaye”.

October 11, 2022