Baraza la Kitaifa la Mitihani humu nchini (KNEC) limewaonya watahiniwa wanaofanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) kuwa waangalifu dhidi ya karatasi ghushi za mtihani zinazosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC Dkt. David Njengere amethibitisha kuwa karatasi za mitihani zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni ghushi na zinalenga tu kuwahadaa wanaofanya mtihani huo.

Njegere aidha ameeleza kwamba mwaka huu baraza hilo limewekeza pakubwa katika kukabiliana na jaribio lolote la wizi wa mitihani, akidhibitisha kwamba visa 46 vya majaribio ya kuiba mtihani vimedhibitishwa kote nchini, huku akieleza kwamba hakuna kisa chochote kilichofanikiwa kuhitilafiana na mtihani kwa kiasi chochote.

Zaidi ya watahiniwa laki tisa wanaendelea na mtihani wa KCSE ambao umeingia juma la pili hii leo.

Wakati huohuo serikali imeweka hatua kali kuhakikisha uadilifu wa mitihani ya kitaifa unazingatiwa. Katibu Mkuu wa Elimu ya Msingi Dkt Belio Kipsang alisema kufikia sasa ni visa vichache vya utovu wa nidhamu ambavyo vimeripotiwa tangu mitihani ilipoanza wiki mbili zilizopita.

Katibu huyo alihusisha hili na mbinu mbalimbali iliyopitishwa katika kusimamia mitihani hiyo na kuwapongeza walimu na vyombo vya usalama kwa juhudi zao za dhati za kuhakikisha mtihani unafanyika bila matatizo.

Akizungumza katika eneo la Kisumu ya Kati Dkt. Kipsang alitoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya mitihani, wakaguzi na maafisa wa usalama kutolegea hadi mitihani yote ikamilishwe.

Share the love
November 13, 2023