Rais Ruto hii leo ametia saini Mswada mpya wa Nyumba za bei nafuu kuwa sheria katika ikulu ya Nairobi. Kutiwa saini kwa sheria hii kunamaanisha kuwa ushuru wa asilimia 1.5 kwa mapato ya wafanyakazi wote nchini umerejea.

Itakumbukwa kuwa awali idara ya mahakama ilifutilia mbali ushuru huu kwa kuwa ulikua ukikusanywa kinyume cha sheria, kabla ya wabunge kuandaa upya mswada huo ambao sasa utaanza kutekelezwa.

Akizungumza katika kikao kilichowaleta pamoja wadau mbalimbali baada ya kusaini mswada huu kuwa sheria, kiongozi wa taifa alionekana kubadili mtazamo wake kwa idara ya mahakama, wakati huu akisema kwamba maagizo ya mahakama yamesaidia katika kuboresha sheria hizi.

Kwa upande wake Naibu wa rais Rigathi Gachagua amesema kuwa mpango huu wa nyumba za bei nafuu utafafanua uongozi wa rais Ruto katika siku za usoni.

Waziri wa ardhi nchini Alice Wahome naye alisifia nafasi za ajira zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa nyumba hizi za bei nafuu.

Aidha ameeleza kwamba wakenya zaidi wa mapato ya chini wamefanikiwa kujipatia kipato kwa njia tofauti katika miradi ya ujenzi wa nyumba hizi.

March 19, 2024