Jengo lenye ghorofa tano liliporomoka katika eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu saa chache baada ya kuhamishwa kwa wapangaji Zaidi ya mia moja kutoka kwa jengo hilo.

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, pamoja na Zimamoto waliongoza shughuli za uokoaji Jumapili baada ya kupokea ripoti kuhusu hatari iliyokuwa ikiwakodolea macho wapangaji hao kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) na OCPD wa Ruiru.Hili ni jengo la pili kuporomoka Kiambu ndani ya wiki moja.

Mnamo Novemba 17, jengo lingine la orofa 5 liliporomoka huko Ruaka, Kaunti ya Kiambu.Wakati huohuo maafisa wa polisi wamefanikiwa kumkamata mmiliki wa jumba lililoporomoka katika eneo la Ruaka na kuwaua watu wawili.

Mshukiwa huyo aliyekuwa akitafutwa tangu mkasa huo ulipotokea, alikamatwa katika uwanja wa ndege wa JKIA akijaribu kuondoka nchini. Kamishna wa kaunti ya kiambu Joshua Nkanatha amesema kuwa mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiambu akisubiri kufikishwa mahakamani.

November 21, 2022