Waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda Moses Kuria ametangaza kuwa serikali itaruhusu uingizaji wa vyakula vya kisaki nchini bila ushuru kwa muda wa miezi sita ijayo. Kuria amedai hatua hiyo inalenga kupunguza uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame unaoendelea.

Rais William Ruto mapema mwezi huu aliondoa marufuku ya uingizaji na upandaji wa vyakula hivyo ambavyo vilianza kutumika tangu 2012, na kuruhusu kilimo cha wazi.Katika kubadili marufuku hiyo iliyodumu kwa miaka 10, rais Ruto alidokeza kuwa vyakula hivyo vitaimarisha usalama wa chakula haswa msimu huu ambapo kiangazi umeshuhudiwa kwa muda mrefu.

Aidha hatua ya kuondolewa kwa marufuku ya utumizi wa vyakula hivyo imeibua hisia tofauti kutoka kwa Wakenya, huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akiwasilisha ombi la kuzuia upandaji na uingizaji wa vyakula hivyo ambavyo anadai ni hatari kwa afya ya binadamu.

November 17, 2022