Wizara ya Elimu imesema kuwa imeziba mianya ya  udanganyifu wakati wa mitihani ya kitaifa na kuongeza kuwa imeweka mikakati ya kuzuia kufichuliwa mapema kwa karatasi za mitihani.

Wakati wa kikao na wanahabari kuhusu utayari wa wizara hiyo, katibu wa elimu ya msingi Belio Kipsang alikiri kwamba kuwapa walimu nafasi ya kuona karatasi za mitihani mapema wanapozichukua asubuhi imekuwa mojawapo ya masuala ambayo yamesababisha visa vya udanganyifu.

Aliongeza kuwa idadi ya vituo vya mitihani imeongezwa ili kupunguza umbali wa kusafiri hatua ambayo anadai itazuia udanganyifu.

Wakati huo huo zaidi ya maafisa 60,000 wa polisi wametumwa katika vituo tofauti vya mitihani kote nchini ili kuhakikisha kuwa mitihani ya KPSEA na KCPE inayoanza Jumatatu, inaendelea bila vikwazo vyovyote.

Haya ni kulingana na Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Dkt. Raymond Omollo, ambaye alisema kuwa usalama pia umeimarishwa katika maeneo tete ya North Rift ambapo visa vya ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya ujambazi vimeongezeka katika miezi ya hivi majuzi.

Kando na hayo alieleza kuwa serikali imeweka vituo vya usalama katika makao makuu ya KNEC, Wizara ya Mambo ya Ndani na Mamlaka ya Mawasiliano ili kufuatilia na kukabiliana visa vyovyote vya ukosefu wa usalama vinavyoweza kujitokeza wakati wa mtihani.

Share the love
October 28, 2023