USALAMA

Wizara ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa imezindua mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa wananchi, kuhusu mapendekezo ya kuongeza ada za kupata nyaraka muhimu ikiwa ni pamoja na kitambulisho cha kitaifa na pasipoti.

Katika taarifa iliyotolewa mapema leo na Katibu Mkuu wa Uhamiaji, Bwana Julius Bitok, wananchi wanakaribishwa kutoa maoni yao hadi tarehe 8 Disemba mwaka huu. Maoni ya wakenya yatazingatiwa katika mchakato wa mwisho wa kutathmini ada mpya, ambazo zinatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka ujao.

Kulingana na mapendekezo yaliyotolewa hapo awali, ada mpya zitakazotozwa zinajumuisha shilingi 1000 kwa wale wanaotaka kubadilisha kitambulisho cha kitaifa kilichopotea. Aidha, wale wanaotarajia kupata kitambulisho cha kitaifa kwa mara ya kwanza watahitajika kulipa ada ya shilingi 300.

Wakenya wameombwa kuwasilisha maoni yao kwenye ofisi za uhamiaji kwenye jumba la Nyayo Jijini Nairobi, afisi za Wakuu wa Mikoa, Makamishna wa Kaunti, au Manaibu Makamishna wa Kaunti. Pia maoni yanaweza kutumwa kwa barua pepe kwa anwani ifuatayo: info.citizenservices@interior.go.ke

Share the love
November 20, 2023