Maafisa wa polisi katika eneo bunge la Mumias kaunti ya Kakamega wanamsaka mwanamume mwenye umri wa miaka 45 kwa jina Simon Mila Alichi ambaye aliwafungia watoto wake wawili katika chumba kimoja na kuwafunga kwa minyororo.

Watoto hao walifungiwa chumbani mchana na usiku, bila chakula.Kulingana na wazazi wa mshukiwa John Mila na Ruth Andayi, wajukuu wao walikuwa wamefukuzwa shuleni na kufungiwa chumbani kimya kimya na baba yao, ambaye alitalikiana na mkewe takriban miaka miwili iliyopita.

Majirani zake, wakiongozwa na Nicholas Nandwa, wanasema mshukiwa huyo a mekuwa akiwaoa wanawake wengine na kuwataliki ndani ya muda mfupi.

Akithibitisha kisa hicho, chifu msaidizi eneo hilo Benson Ochango aliwanyooshea kidole cha lawama majirani kwa kukosa kuripoti tukio hilo kwa wakati.

Mila alitoroka eneo hilo baada ya kufumaniwa na maafisa wa usalama.Watoto hao wamepelekwa katika makao ya watoto huko Mumias, wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu yeyote atakayepewa malezi.

May 24, 2023