Fisi awavamia wananchi Naikarra

Watu wanne wa familia moja katika kijiji cha Olopilukunya, eneo la Naikarra katika kaunti ndogo ya Narok magharibi, wanauguza majeraha mabaya baada ya kuvamiwa na fisi usiku wa kuamkia leo.

Jackson Masago, ambaye ni mmoja wa jamaa wa familia hiyo, ameeleza kuwa fisi huyo aliingia ndani ya nyumba mwendo wa saa tatu usiku, wakati jamaa hao walikuwa wanakula chajio, na kuanza kuwashambulia. Waliojeruhiwa na kung’atwa na fisi huyo ni pamoja na bikizee mmoja aliyeachwa na majeraha kwenye titi moja na kwenye mkono, kina mama wawili waliopata majeraha ya mgongo, na msichana mmoja mwenye umri wa miaka saba aliyeachwa na majeraha ya mkono.

Shughuli za kuwasaidia waliovamiwa kupata huduma za matibabu zimekumbwa na changamoto kutokana na barabara mbovu katika eneo hilo, hali ambayo imechangiwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha. Familia hiyo imetoa wito kwa viongozi wa eneo hilo kuwasaidia kupata usaidizi wa haraka ili kuokoa maisha yao.

April 26, 2024