Ajali

Watu sita wameaga dunia na wengine saba kujeruhiwa vibaya katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea eneo la Silanga kwenye barabara kuu ya Narok kuelekea Mulot. Ajali hiyo imetokea saa tatu usiku siku ya Jumapili na imehusisha magari mawili, gari aina ya Toyota Sienta lenye abiria sita na gari lingine aina ya Subaru Forester.

Kulingana na ripoti ya maafisa wa usalama, dereva wa gari la Subaru Forester alikuwa akielekea upande wa Narok kutoka Mulot na alijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake kabla ya kugongana uso kwa uso na Toyota Sienta iliyokuwa ikielekea upande wa Mulot kutoka Narok.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Narok ya Kati, John Momanyi, alithibitisha ajali hiyo na kusema kuwa watu wote waliokuwa katika gari aina ya Toyota Sienta waliaga dunia papo hapo. Dereva wa Subaru Forester pia alikimbizwa katika hospitali moja ya kibinafsi baada ya kulalamikia maumivu ya kifua.

Miili ya walioaga dunia ilipelekwa kwenye makafani ya hospitali ya Rufaa mjini Narok kwa ajili ya uhifadhi na upasuaji zaidi.

April 22, 2024